Saturday, November 07, 2009

Mshahara wa Kondic aulizwe Manji

UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema hauhusiki na ulipaji wa mshahara wa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Dusan Kondic na anayewajibika na suala ni mfadhili mkuu, Yusuph Manji kama ilivyokuwa katika makubaliano yao.

Kondic ambaye yupo nje ya nchi kwao mara baada ya kuachia ngazi ya kuendelea kukifua kikosi cha Jangwani bado anaidai klabu hiyo mshahara wake wa miezi mitatu ambao hakulipwa.

Afisa habari wa klabu ya Yanga, Louis Sendeu alisema wao kama uongozi hawawajibiki na ulipaji mshahara kwa kocha huyo na hiyo ni jukumu la mfadhili wao ambaye katika mkataba wake ulionyesha yeye mlipa wake atakuwa mfadhili wa klabu hiyo.

Alisema ni kweli kocha huyo anadai kiasi cha shilingi milioni 30 ambazo ni za miezi mitatu, lakini wao hawahusiki katika hilo na hivyo kumwachia mfadhili , Manji kama ilivyokuwa awali.

"Katika jukumu la kumlipa kocha sisi kama uongozi hatuhusiki kwani kocha alipokuja kusaini mkataba ilisaini kuwa analipwa na mfadhili na sisi katika hilo hatuhusiki hivyo hiyo si kazi yetu sisi na endepo atarejea kwa ajili ya kuchukua malipo yake anatakiwa kwenda kwa muhusika na si uongozi,"alisema Sendeu.

Klabu ya Yanga kwa sasa inanolewa kocha Kostadin Papic ambaye amechukua nafasi ya Kondic aliyeiacha klabu hiyo

MWANANCHI

Saturday, October 31, 2009

Tumelala 1-0

Bao pekee la mchezo liliofungwa na Musa Hassan Mgosi leo limetutoa katika Uwanja wa Taifa vichwa chini baada ya Simba kuendeleza wimbi lake la ushindi na sasa kufikisha pointi 30 katika michezo 10.
Mgosi alifunga bao hilo baada ya kupewa pasi na Danny Mrwanda katika dakika ya 26. Hata hivyo Mrwanda hakumaliza mchezo huo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 68.
Hongera kwa walioshinda, ligi inaendelea.
Yanga vs Simba

Macho na masikio ya maelfu ya mashabiki wa soka nchini leo yataelekezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara kati ya vigogo vya soka hapa nchini Simba na Yanga.

Huo utakuwa ni mchezo wa pili kwa vigogo hivyo kukutana ndani ya mwaka huu, ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni Aprili 19 katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja huo na timu hizo kwenda sare ya 2-2, ambapo Yanga ilikuwa na jukumu la kusawazisha.

Mchezo wa leo utakuwa na umuhimu mkubwa kwa Yanga kutokana na ukweli ina changamoto kadhaa za kukabiliana nazo.

Kocha mpya, Kostadin Papic aliyechukua mikoba kutoka kwa Dusan Kondic atakuwa anakalia benchi la timu hiyo kwa mara ya kwanza wiki tatu zilizopita.

Pia Yanga yenye pointi 18 itakuwa na kibarua cha kupunguza kasi ya Simba, ambayo inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 27 baada ya kushinda mechi zake tisa za mwanzo.

Kutokana na ukweli kuwa ikipoteza mchezo huo ina maana itazidi kutoa mwanya kwa Simba kuzidi kupaa katika msimamo wa ligi hiyo. Yanga itakuwa fursa kwao kuendeleza ubabe wa kuifunga Simba kwa mara ya pili kwenye uwanja huo kama ilivyofanya katika raundi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu uliopita, ambako Yanga ilishinda bao 1-0, Oktoba 26,2008.

Katika mchezo huo, Simba itakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha wanaendeleza wimbi la ushindi kwenye michezo yake ya ligi pamoja na kutaka kuweka rekodi mpya ya kushinda michezo 10 mfululizo.

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Yanga, Kostadin Papic alisema kuwa mara baada ya kukirekebisha kikosi chake ana matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo.

Kwa upande wake, kocha wa Simba, Patrick Phiri aliweka wazi kuwa anachohitaji ni pointi tatu kutoka kwa Yanga na uhakika wa kuzipata pointi hizo anao.

Tuesday, October 27, 2009

Tibaigana awafungulia akina Maftah

WACHEZAJI Amir Maftah na Moses Odhiambo wa Yanga, wako huru kuichezea timu yao kwenye mpambano wa Jumamosi dhidi ya Simba baada ya kufutiwa kifungo cha kukosa mechi tatu na faini ya shilingi 500,000 baada ya kikao cha kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kushindwa kuwasilishwa kwa aina ya matusi waliyotukanwa na wachezaji hao ni moja ya sababu za kuachiwa huru na kufutiwa faini ambayo ilitakiwa kulipwa na wachezaji hao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa kamati hiyo Kamishna wa Polisi Mstaafu, Alfred Tibaigana alisema kamati yake imeshindwa kugundua kosa na kutoa maamuzi ya kuwapa uhuru wachezaji hao kwa kushindwa kugundua sababu halisi ya makosa waliyoshitakiwa.

''Hukumu inaonyesha kuwa wachezaji hao walimtukana msaidizi wa mwamuzi wa kwanza mara baada ya mpira kumalizika na taarifa hizo zikaandikwa kwa taarifa ya kamisaa,''alisema Tibaigana.

''Hukumu ambayo bado haina uhakika kwa kuwa walishindwa kuandika aina ya matusi ambayo yalitukanwa na wachezaji hao, na sisi kama kamati hukumu za namna hiyo huwa tunazihukumu kwa kumpa haki mshatakiwa kwa kuwa zinakuwa za shaka kwa kutokamilika.

''Itakuwa bora yanapotokea matatizo kama hayo , basi waamuzi wanapoandika ripoti zao wanatakiwa kuandika aina ya matusi ambayo wanatukanwa kwa kuwa wao ni binadamu na tukio kama hilo halikuwa na ushahidi,'' alieleza Kamanda Tibaigana.

Alisema wao kama kamati ya mashindano wamewaachia huru wachezaji hao tangu kufanyika kwa kikao hicho kilipokutana na kubaini kushindwa kwa waamuzi na kamisaa kuweka bayana matusi kutambua makosa kazi ambayo wamewaachia TFF kama itakatwa rufaa nyingine.

Kutokana na uamuzi huo, Maftah na Odhiambo waliotiwa hatiani na kupewa adhabu na faini hiyo wakidaiwa kumtukana mwamuzi siku ya mchezo baina ya Yanga na Azam FC mchezo uliomaliza kwa suluhu ya bao 1-1, wameondolewa kifungoni.

Sunday, October 25, 2009

Msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom

Yanga vs Moro Utd

Yanga leo inajitupa kwenye uwanja wa Uhuru kupambana na Moro United katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania.

Mechi imemalizika kwa Yanga kuichapa Moro United 1-0. Bao la Yanga limefungwa na Nurdin Bakari katika dakika ya 32.

Kwa ushidi huo, Yanga ipo katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kwa kujikusanyia jumla ya pointi 18.

Thursday, October 22, 2009

Odhiambo, Maftah kuikosa Simba
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limewafungia wachezaji wake Amir Maftah na Moses Odhiambo wasicheze mechi tatu za Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.

Wachezaji hao 'wamekwenda jela' zikiwa zimebaki siku kumi kabla ya mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga.

Timu za Yanga na Simba zinatarajiwa kumenyana Oktoba 31 katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ofisa Habari wa TF, Florian Kaijage, amewaeleza waandishi wa habari jana kuwa,kikao cha Kamati ya Mashindano ya shirikisho hilo kimetoa uamuzi huo Jumatatu wiki hii.

wachezaji hao wamepatikana na hatia ya kumshambulia kwa maneno mwamuzi msaidizi namba moja aliyechezesha mechi ya Yanga na Azam Oktoba 17 na kutaka kuingia chumba cha waamuzi kufanya fujo.

Wachezaji hao pia wametozwa faini ya sh.500,000 kila mmoja,Yanga imetozwa kiasi hicho hicho baada ya mashabiki wake kumrushia mwamuzi msaidizi namba moja chupa za maji, mawe na kusababisha mchezo kusimama kwa dakika moja.

Msemaji wa Yanga, Loius Sendeu alisema jana kuwa watakutana kujadili cha kufanya.

“Inashangaza sana uamuzi huu, lakini tutakutana haraka iwezekanavyo na kuamua tuchukue hatua gani,” alisema Sendeu.

...........Cirkovic mgonjwa
Sendeu pia alisema, kipa wao wa kutumainiwa,Obrein Cirkovic,juzi aliugua ghafla, akalazwa katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam, amepata nafuu, na ameruhusiwa jana.

“Hatujajua hali yake itakuwaje, lakini tunaomba apate nafuu ili aweze kuitumikia Yanga kama kawaida,” alisema Sendeu.

Saturday, October 17, 2009

Yangaic vs Azam FC


Kocha mpya wa Yanga Kosta Papic leo anapata mtihani wake wa kwanza kwa kupambana na Azam FC katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Uhuru.
Yanga inakumbana na moja ya timu ngumu katika ligi hiyo kwani ina wachezaji kadhaa ambao wanaweza kusumbua katika mchezo wa leo.

Mshambuliaji John Boko wa Azam ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji katika ligi hiyo. Timu hiyo pia ina beki wa kutegemewa wa Taifa Stars Salum Sued pamoja na viungo wazoefu kama Shaban Kisiga. Azam inanolewa na kocha msaidizi wa zamani wa Taifa Stars, Itamar Amorin.
Hata hivyo kwa vyovyote itakavyokuwa, wachezaji wa Yanga hawatataka kumwangusha kocha wao mpya kutoka Serbia ili aweze kuwa na mwanzo mzuri katika kukisuka kikosi hicho.
Yanga na Azam zote zina pointi 14.
Katika michezo mingine ya ligi hiyo, Majimaji itaikaribisha Manyema FC ya Dar, Prisons itakuwa nyumbani dhidi ya Toto Africa.
Matokeo ya mechi za leo:
Yanga vs Azam 1-1
Prisons vs Toto Africa 1-1
Majimaji vs Manyema 0-0